Usikasirike!

Ninaomba maisha yenu yajazwe upendo na baraka za Mungu. Sasa ningependa kushiriki nanyi neema kupitia ujumbe wenye kichwa “Usikasirike!” Mwaka mpya unapofika, kila mtu hutamani kuondoa mambo yote yanayomsumbua na kumlemea na kutarajia yatokee mambo mazuri tu.

Kwa nia hiyo, ninaomba mtii na kulitenda Neno la Mungu kikamilifu, na kufanikiwa katika kila jambo, zikiwemo afya, fedha, heshima na mamlaka. Upendo huufanya moyo wa mtu uwe hai na wenye matumaini. Kinyume chake, hasira humfanya awe mtu hasi na mwenye huzuni. Mtego mkuu ambao adui Ibilisi huwawekea watoto wa Mungu ni chuki na hasira ya haraka. “Kukasirika” hakumaanishi tu “kukasirika sana,” “kupaza sauti na kusema maneno machafu,” au “kutenda kwa ukatili.”

Kukasirika kunatia ndani pia kukunja uso, kupauka na kuzungumza kwa ukali. Hii ni kwa sababu hisia za chuki, hasira ya haraka, kiburi na kinyongo zilizofichika ndani ya moyo hudhihirika. Hata hivyo, usimhukumu mtu kuwa amekasirika kwa kuangalia sura yake tu. Mungu pekee ndiye anayeweza kuona moyo wa kila mtu. Kwa mfano, huenda mtu akionekana amekasirika kumbe hana hasira hata kidogo.

Huenda kwa asili yake sauti yake huwa kubwa, ya ugomvi, ya kushambulia au ya hasira. Basi, ufanye nini ili usikasirike? Kwanza, ondoa hisia mbaya zinazochochea hasira moyoni mwako. Bila shaka, huwezi kuondoa hisia zote mbaya, kama chuki, kiburi na karaha, kwa siku moja; kwa hiyo unapaswa kujitahidi kila siku. Pili, vumilia unapokutana na hali zinazochochea hasira yako.

Usipovumilia na badala yake ukapigana na mwingine, jambo hilo litasababisha ugomvi mkubwa zaidi au uadui kati yenu. Ingekuwa jambo la kufurahisha kiasi gani kama ungeweza kuondoa kwa nguvu na juhudi zako mwenyewe hisia mbaya zinazochochea hasira! Lakini juhudi zako pekee haziwezi kukuondolea kabisa hisia mbaya za aina mbalimbali, kama chuki, kiburi na kero. Ndiyo maana unahitaji nguvu za Mungu. Nguvu zake hupewa unapomwomba kwa bidii na kwa sauti.

Kupitia maombi hayo ya bidii unaweza kubadilishwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu na neema na nguvu za Mungu. Kadiri unavyoondoa hisia mbaya zinazochochea moyo wako, ndivyo moyo wako unavyojazwa wema, upendo na upole. Hata mwingine akikukera, moyo wako hautatikisika bali utakuwa mtulivu kama ziwa lisilo na mawimbi. Kama 1 Wakorintho 13:4 inavyosema, upendo huvumilia na hufadhili.

Mstari unaofuata, mstari wa 5, unasema kwamba upendo haukasiriki. Kwa hiyo, vua kila kitu kinachochochea hasira moyoni mwako kama unavyovua nguo zilizochakaa, na uvae mavazi mapya ya wema na upendo. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life